Klabu ya Namungo ya Ruangwa mkoani Lindi imemtangaza Juma Mgunda kuwa Kocha wao mkuu kuchukua nafasi ya Mwinyi Zahera ambaye amepangiwa majukumu mengine ndani ya klabu hiyo
Klabu ya Namungo ya Ruangwa mkoani Lindi imemtangaza Juma Mgunda kuwa Kocha wao mkuu kuchukua nafasi ya Mwinyi Zahera ambaye amepangiwa majukumu mengine ndani ya klabu hiyo. Mgunda anauzoefu wa kufundisha ligi kuu Tanzania bara baada ya kufundisha timu mbalimbali zinazoshiriki ligi kuu Tanzania.
Mgunda atasaidiana na Ngawina Ngawina, Shedrack Nsajigwa na Vladmir Niyonkuru kwenye majukumu yake mapya ndani ya Namungo. Timu hiyo ya yenye makao makuu yake mkoani Lindi imeanza vibaya msimu huu wa ligi kuu Tanzania inashika nafasi ya 13 baada ya kucheza michezo 7.
Namungo imeshinda michezo 2 kati ya 7 iliyocheza msimu huu wa 2024-2025 ikiwa na alama 6 pekee huku ikiwa imefunga idadi ya goli 4 na kuruhusu goli 8.
Kikosi hiko cha Wauaji wa kusini kinawachezaji wengi wenye uzoefu wa ligi kuu ya Tanzania bara ambao wamewahi kuhudumu kwenye timu mbalimbali nchini. Medie Kagere, Beno Kakolanya ,Jacob Masawe, Rafael Daud na Erasto Nyoni. lakini matokeo chanya yamekuwa hadimu kupatikana msimu huu.
Mgunda kama anavyofahamika kwa jina Guardiola Mnene na Wadau wa Soka Tanzania alipata mafaniko makubwa akiwa na kikosi cha Wekundu wa Msimba kwa upande wa Wanawake aliiongoza timu hiyo kushinda ubingwa wa ligi kuu ya Wanawake Tanzania. Pia aliwahi kufundisha akiwa Kocha Mkuu timu ya Simba SC ya Wanaume na kuiongoza kuingia hatua ya makundi klabu Bingwa barani A frika.
Kocha huyo anayependa boli litembee kwenye timu zake anazofundisha amewahi kufundisha Coastal Union ambayo aliiongoza kucheza mchezo wa fainali ya kombe la Shirikisho Tanzania dhidi ya Yanga ambapo timu hiyo ya Tanga ilipoteza mchezo huo kwa changamoto ya mikwaju ya penati.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Wana Mangushi anatarajiwa kuanza kibarua chake rasmi siku ya Ijumaa Oktoba 25, ambapo ataiongoza klabu ya Namungo kukabiliana na Waajiri wake wa zamani Simba SC mchezo utakaochezwa uwanja wa KMC Complex.