Watuhumiwa hao ambao ni watumishi mikopo wa OYA walifikishwa mahakamani mbele ya Hakimu Emmael Lukumai na kusomewa shitaka na Wakili wa Serikali Monica Mwela.
Kesi hiyo namba 29566 ya mwaka 2024 imesomwa kwa shtaka la mauaji ya kukusudia na hawakutakiwa kujibu lolote kwani mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo.
Waliofikishwa mahakamani ni Abdallah Felix Wendelin (32), Christopher Kitanda (26), Emmanuel Olala wote wakazi wa Janga Mlandizi na Dastan Charles (23) mkazi wa Kilangalanga Mlandizi wilayani Kibaha.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi mkoa wa Pwani kufuatia tukio la Mfaume kuuawa ilieleza kuwa, "Tarehe 7,10,2024 katika kitongoji cha Mbagala, wilaya ya kipolisi Mlandizi,mkoani Pwani watu wanne ambao ni wafanyakazi wa kampuni ya mikopo ya OYA walifika nyumbani hapo Kwa lengo la kudai fedha za marejesho ya mkopo kwa mke wa Juma Saidi Mfaume aitwaye Khadija Ramadhani, baada ya kufika nyumbani kwa Juma Mfaume aliwaeleza kuwa mkewe hayupo lakini watuhumiwa hao walilazimisha kuingia ndani kwa nguvu huku wakimshambulia sehemu mbalimbali za mwili wake kwa kutumia fimbo na baadaye alianguka chini na kupoteza fahamu,"