Saturday , 17th Aug , 2024

Rais wa Jamhuri ya Zambia, Hakainde Hichilema ameihakikishia ushirikiano Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati huu inapotarajia kukabidhiwa jukumu la uenyekiti wa Asasi ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC (SADC Organ on Politics, Defence and Security)

 

Kadhalika, ameshukuru kwa ushirikiano alioupata wakati wa uongozi wake na pia ameonesha kuwa na imani na Tanzania katika kupokea jukumu la unyekiti wa Asasi ya SADC Organ Troika.

“Nipende kumhakikishia ushirikiano dada yangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na wasaidizi wake, pia nina imani utaiongoza Organ na kuifikisha katika hatua ya juu ya mafanikio kama ambavyo umekuwa ukifanya katika majukumu mengine uliyoaminiwa” Mhe. Hichilema.

Hayo yamejiri wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi hiyo ya SADC Organ Troika uliofanyika tarehe 16 Agosti, 2024 Harare, Zimbabwe nakuhudhuria na Mhe. Hichilema Rais wa Jamhuri ya Zambia na Mwenyekiti wa sasa ambaye ameshiriki kwa njia ya mtandao.

Mbali na Mhe. Hichilema Mkutano huo pia umeudhuriwa na Mhe. Nangolo Mbumba Rais wa Namibia Namibia na Mwenyekiti wa Organ aliyemaliza muda wake na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti ajaye wa Asasi hivyo kukamilisha safu ya nchi zinazohunda Utatu huo.

Aidha, katika hotuba wakati wa kufungua na kufunga mkutano Mhe. Hichilema amewashukuru wajumbe wa mkutano huo kwa kutumia muda wao na rasilimali zao kuhudhuria na kushiriki kikamilifu katika mijadala mbalimbali yenye maslahi ya kanda.

“Ni matumaini yangu kuwa agenda zilizowasilishwa mbele yetu zitajadiliwa kwa tija na kwa maslahi ya pande zote kwa ajili ya ustawi wa Jumuiya na watu wetu” alisema Mhe. Hichilema.

Hivyo, ni muhimu kuwa tayari kuonesha umoja na nia ya kufanikiwa kwa pamoja katika kuijenga jumuiya yenye amani na usalama hali ambayo itachangia kukuza uchumi kupitia shughuli za biashara na uwekezaji kwenye kanda.
Pia, alitoa shukrani za kipekee kwa Jamhuri ya Namibia kwa kipindi ambacho imeongoza kupitia Hayati Rais Hage Geingob na Rais wa sasa Mhe. Dkt. Nangolo Mbumba, sambamba na Sekretarieti ya SADC kwa usikivu, uvumilivu na uongozi wa mfano wa Bw. Elias Magosi ambaye pamoja na timu yake wamekuwa wakifanya kazi bila kuchoka kuratibu kufanyika kwa mikutano hiyo.

Vilevile akaeleza kuwa utatu wa asasi hiyo ni utaratibu mzuri wa kuendesha taasisi yoyote yenye lengo la kufikia mafanikio kwakuwa, inaruhusu muendelezo wa utekelezaji wa masuala mbalimbali ya kikanda na kuhifadhi kumbukumbu ya masuala mbalimbali ili hurahisisha ufuatiliaji na maamuzi.

Tanzania inatarajia kukabidhiwa nafasi ya uenyekiti wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC (SADC Organ on Politics, Defence and Security) katika Mkutano wa Kawaida wa 44 wa Wakuu wa Nchi na Serikali utakaofanyika tarehe 17 Agosti, 2024 Harare, Zimbabwe.

Pamoja na masuala mengine mkutano huo wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC Organ Troika umepitia na kujadili hali ya ulinzi na usalama katika kanda, hali ya ulinzi na usalama katika Falme za Eswatini na Lesotho, hali ya ulinzi na usalama katika jimbo la Cabo Del Gado na hali ya ulinzi na usalama Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.