Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe Dkt. Doto Biteko
Dkt. Biteko ameyasema hayo leo 11 Agosti, 2024 jijini Dar es Salaam wakati alipofanya ziara ya kutembelea vituo vya umeme vya Ubungo I, Ubungo II, Ubungo III pamoja na kituo cha kudhiti mifumo ya umeme wa gridi yaani Grid control Centre.
Dkt. Biteko ameitaka TANESCO kuhakikisha matengenezo ya miundombinu ya umeme yanakuwa endelevu ili Watanzania wapate umeme wa uhakika.
"Kwa kweli namshukuru Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa msukumo wake mkubwa katika sekta ya nishati na sisi kama Wizara kupitia TANESCO tutaendelea kuhakikisha Watanzania wanapata umeme wa uhakika," Amesema Dkt. Biteko
Amesema kwa sasa kuna ziada ya umeme na ndio maana matengenezo yanaweza kufanyika kwenye mitambo katika vituo vya Kidatu, Kihansi na Mtera na hivi karibuni TANESCO itakamilisha matengenezo kwenye laini za Mikoa ya Kaskazini ili kuimarisha hali ya upatikanaji wa umeme ambapo amewashukuru wananchi wa mikoa hiyo kwa uvumilivu wao katika kipindi chote cha matengenezo.
Amesisitiza kuwa, kwa sasa hali ya upatikanaji wa umeme ni ya kuridhisha hasa ikizingatiwa kuwa mradi wa bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere unaendelea vizuri na tayari mashine tatu zimeshaungwa kwenye gridi ya Taifa na mashine ya nne inatarajiwa kuingizwa mwezi huu na kwamba tayari mashine tatu za mradi wa Rusumo zinafanya kazi.