Wednesday , 10th Jul , 2024

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema tayari maelekezo yametolewa kwa Wizara ya Mambo ya
Ndani ya Nchi kuhakikisha inaharakisha upatikanaji wa vitambulisho vya Taifa ili kuondoa adha wanayopitia wananchi wa Kigoma na maeneo mbalimbali
nchini.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akizungumza na wananchi wa eneo la Mnanila akiwa ziarani mkoani Kigoma. Amesema kukosekana kwa vitambulisho hivyo kunawanyima fursa mbalimbali wananchi hao ikiwemo kukosa ajira katika miradi inayotekelezwa mkoani humo.

Makamu wa Rais amesema serikali inaendelea kutekeleza kikamilifu miradi ya ujenzi wa barabara kiwango cha lami ili kuunganisha mkoa huo na mikoa mingine ya Tanzania ambapo kwa upande wa barabara ya Tabora – Kigoma ni kilometa 51.1 pekee zimesalia kukamilika na zinatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Machi 2024. Pia amesema kwa upande wa barabara ya Kagera – Kigoma ni kilometa 16 pekee zimesalia kuunganisha mikoa hiyo.

Makamu wa Rais ameusisitiza uongozi wa Mkoa wa Kigoma kushughulikia changamoto ya kukataliwa kupata ajira za kawaida katika mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) kwa sababu ya ukosefu wa vitambulisho vya Taifa. Amesema suala hilo linapaswa kushughulikiwa kwa wananchi kupata ajira hizo kwa kutumia vitambulisho mbadala kama vile leseni na vitambulisho vya kupigia kura. Ameongeza kwamba wananchi wataweza kulinda vema miradi hiyo kama watashiriki katika ujenzi wake.

Halikadhalika Makamu wa Rais amesema kukamilika kwa uwanja wa ndege wa kisasa unaojengwa mkoani Kigoma kutafungua fursa ya utalii na biashara mkoani humo. Pia amesema Mkoa huo unatarajiwa kuondokana na changamoto ya kufuata huduma za afya katika maeneo mengine ya nchi kwa kuwa serikali inatarajia kujenga Hospitali ya Kanda ya Magharibi katika eneo la Ujiji mkoani humo.