Friday , 17th May , 2024

Serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) imepanga kununua mitambo mingine 10 ya uchorongaji kwa ajili ya kusaidia wachimbaji wadogo nchini.

Hayo yamesemwa leo Mei 17, 2024 na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde aliposhiriki zoezi la kuwakabidhi leseni Chama cha Wanawake Wachimbaji mkoani Simiyu (TAWOMA) katika Kata ya Dutwa wilayani Bariadi.

"Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametupatia fedha za kuongeza mitambo mingine 10 ya uchorongaji kupitia STAMICO na ametuelekeza kuwa mitambo hiyo ikifika nchini Mwezi Agosti au Septemba, 2024 mitambo miwili tuiweke mahsusi kwa ajili ya wachimbaji wadogo wanawake na vijana, ni dhamira ya serikali kuwawezesha wachimbaji wadogo kwa kuwapatia vifaa na kuimarisha shughuli zao ili ziwanufaishe watanzania," amesema Waziri Mavunde.

Pia, Waziri Mavunde amemuagiza Afisa Madini Mkazi mkoa wa Simiyu, Mayigi Nchagwa Makolobelo, kusimamia vijana na wanawake ili waunde vikundi, ili katika maeneo yanayorejeshwa serikalini kwa zoezi la ufutaji wa leseni vikundi hivyo vipatiwe maeneo ya uchimbaji.