Thursday , 2nd May , 2024

Vijana wanaopata mafunzo ya jeshi la kujenga Taifa JKT wametakiwa kuwa walinzi wa miradi ya maendeleo ikiwemo miradi mikubwa inayotekelezwa na serikali kote nchini ili iweze kuwa na tija kwa taifa ikiwa ni pamoja na kupambana na wale wote wanaobeza miradi hiyo. 

Wahitimu wa Mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa JKT

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa Tanga Balozi Dkt. Batilda Buriani wakati akifunga mafunzo ya awali ya kijeshi ya vijana wa kujitolea oparesheni miaka 60 ya jeshi la kujenga Taifa katika kikosi cha 838 Maramba JKT. 

Balozi Dkt Batilda Buriani amesema ni jukumu la vijana kuyaelezea mazuri yote yanayofanywa na serikali katika miradi mbalimbali ya kimaendeleo na iwapo wataona serikali inasemwa vibaya basi wanajukumu la kuelezea ukweli kwa watanzania. 

"Wewe kijana unapoona serikali inasemwa vibaya na unajua ukweli na upo katika ukurasa huo nyinyi ndio wasemaji wa serikali elezea ule ukweli unaoujua usiuache ubaya ukisemwa sana basi watu wanadhani ni ukweli kama kuna lile ambalo unalijua linyooshe na kama hulijui tuulizeni tutawaambia tusaideni kuusambaza ukweli wananchi wajue ukweli ni upi,  "alisisitiza Dkt Batilda. 

Aidha Balozi Dkt Batilda aligusia suala la ndoa za jinsia moja na kuwataka vijana kujiepusha nalo na kwamba jambo hilo litawakosesha vijana sifa ya kuwa askari na hatimaye kushindwa kufikia ndoto zao. 

Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkuu wa majeshi nchini Brigedia Jenerali Abubakary Charo amewaomba vijana wote ambao hawapati fursa ya kujiunga na jeshi la kujenga Taifa kuwa avumilivu wakati serikali ikiendelea kuweka  mazingira rafiki ili kila mwenye sifa aweze kujiunga. 

"Wale wa mujibu wa sheria,  wale wanaomaliza kidato cha sita lakini na hawa wa kujitolea wanaokuwa na nia ya kujiunga na jeshi la kujenga Taifa lakini hawakupata nafasi wasije wakafikiri kwamba wametengwa wasifikiri kwamba wamenyimwa fursa hapana lengo ni vijana wote wapite katika mafunzo haya hivyo ni imani yangu kamba ipo siku wale vijana wanaomaliza kidato cha sita wote wataweza kuchukuliwa na kufanya mafunzo haya ya JKT, "alisema Brigedia jeneral Charo. 

Naye Mwakilishi wa Jeshi la kujenga Taifa JKT Kanal Ernest Elias Kaponda amesema mafhnzo hayo waliyoyapata vijana hao wamekuwa tayari kulitumikia na kulilinda Taifa lao popote watakapokwenda kwakuwa wamefahamu dhana ya uzalendo,  umoja , ushirikiano,  mshikamano,  ukakamavu na kujiamini hivyo amewataka kutumia elimu hiyo katika kutatua changamoto mbalimbali pasipokuvunja sheria na taratibu za nchi. 

Kamanda kikosi cha 838 Maramba JKT Luteni Kanal Ashraf Bakary Hassan amesema vijana hao waliotokea Mikoa mbalimbali hapa Nchini wamefundishwa katika viwango vinavyokubalika na ambavyo vimepitishwa na jsshi la kujenga Taifa hivyo ana imani vijana hao watakuwa mfano wa kuigwa katika jamii na watakuwa tegemeo kubwa kwa Taifa. 

Mafunzo hayo ya vijana wa kujitolea oparesheni miaka 60 ya jeshi la kujenga Taifa yamehusisha vijana kutoka mikoa mbalimba nchini ambapo walianza mafunzo hayo tarehe 27 mwezi desemba mwaka jana na kuhusisha vijana 600 waliohitimu katika kikosi cha 838 Maramba KJ.