Wednesday , 6th Mar , 2024

Mkutano Mkuu wa ACT Wazalendo umemchagua Bi. Dorothy Semu kuwa kiongozi wa Chama hicho akichukua nafasi ya Zitto Kabwe ambaye amemaliza muda wake wa uongozi kwa mujibu wa katiba.

Zoezi la upigaji kura kuchagua nafasi ya Kiongozi wa Chama, Mwenyekiti wa chama, Makamu Mwenyekiti wa chama Bara na Zanzibar.

Bi. Dorothy ameshinda nafasi hiyo kwa kupata kura 534 sawa na asilimia 65.7% ya kura zote akimzidi mshindani, Mbarala Maharagande aliyepata kura 184 sawa na asilimia 34.3%.

Akizungumza wakati akitoa neno la shukrani, Bi. Dorothy amesema chama hicho kimeonyesha ukomavu wa kidemokrasia na kujenga chama cha kipekee ambacho kimeamua kudumisha demokrasia kuanzia ndani ya chama na kuandaa vijana na makundi mengine ya kijamii kushiriki siasa. 

"Viongozi wa ACT Wazalendo tunatakiwa tusiondoe macho yetu kwenye changamoto za kila siku zinazowaumiza, kuwasumbua na kuwabugudhi Watanzania" alisema Dorothy Semu, Kiongozi Mkuu wa ACT Wazalendo. 

Akizungumzia jukumu lao kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mtaa na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, Bi. Dorothy amewaelekeza viongozi wa chama hicho kuhamasisha na kuhakikisha wanachama wao wanashiriki kikamilifu katika kujiandikisha kupiga kura katika chaguzi hizo. 

Aidha katika Mkutano huo, Othuman Masoud amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa chama baada ya kupata kura 539, sawa na asilimia 99.6% ya kura zote zilizopigwa.

Kwa upande wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti upande wa Bara Isihaka Mchinjita amechaguliwa kwa kura 517 sawa na asilimia 96.1, huku nafasi ya Makamu Mwenyekiti Zanzibar ikienda kwa Ismail Jussa aliyeshinda kwa kura 509 sawa na asilimia 99.6% ya kura zilizopigwa.