Sunday , 25th Feb , 2024

Naibu Waziri wa Afya Dkt Godwin Mollel amesema Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameagiza majeruhi wote waliotokana na ajali iliyoua watu 25 mkoani Arusha watibiwe bure

Dkt Godwin Mollel  amesema hayo leo Februari, 25, 2024 alipowajulia hali  majeruhi wa ajali hiyo iliyohusisha magari manne eneo la Ngaramtoni, Mkoani Arusha waliolazwa katika  Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mount Meru. 
Dkt.  Mollel amesema majeruhi wote wanaendelea vizuri na mmoja  ndo kapewa  Rufaa ya kwenda  hospitali ya Rufaa ya Kanda KCMC Mkoani Moshi.

"Rais Samia Suluhu Hassan ametuelekeza  majeruhi wote  wa ajali  hii  kupatiwa matibabu bila  kulipa  gharama zozote",

Dkt. Mollel ametoa  wito  kwa wananchi wa mkoa wa Arusha na watanzania kwa  ujumla kuwa watulivu wakati  wakiendelea  kuwatibia  majeruhi  na kwa wale  waliopoteza  ndugu  zao  utaratibu  wakupatiwa miili  unaandaliwa  na wataalamu. 

Aidha  Dkt. Mollel kwa niaba  ya Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amewashukuru na kuwatia  moyo  watumishi wa afya  katika hospitali  ya Rufaa ya Mkoa Mount Meru  kwa kazi  nzuri  waliofanya  katika  kuwahudumia majeruhi wa ajali  hiyo

 Kwa upande wake mmoja wa majeruhi Raia  wa  Togo, Apelo Apeto (32) ameishukuru Serikali ya Tanzania  kwa  ubora wa Huduma waliompatia  na anayoendelea  kupatiwa  hospitalini  hapo.

"Kwa ajali  hii   ningekuwa  nchini  kwetu tayari  ningekuwa  nimepoteza  maisha kwani  kule  bila kilipia  huduma  za matibabu  hupatiwi  huduma, lakini  kwa  Tanzania walivyowakarimu na weledi  wameweza  kuokoa maisha  yangu  mpka sasa naendelea  vizuri na naweza  kuongea ", ameeleza Raia  wa  Togo

 
Raia huyo amesema alikuja  nchini  Tanzania  kwa semina  ya mafunzo  ya uongozi  iliyokuwa  ikifanyika  mkoani  hapo na baadaye  wakaenda  kufanya  utalii  wa kuangalia kabila la wamasai wakati  wanarudi  ndo wakapata  ajali  hiyo.

Awali akizungumza na vyombo vya Habari Kamishna wa Polisi Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi CP Awadhi Juma Haji amesema Watu 25 wamefariki dunia huku wengine 21 wakijeruhiwa katika ajali iliyotokea maeneo ya Ngaramtoni kibaoni ikihusisha Lori na magari mengine madogo matatu Wilaya ya Arumeru Mkoa wa Arusha.