Friday , 16th Feb , 2024

Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga, amesema kwamba changamoto ya mgao wa umeme nchini itaisha rasmi mwezi wa tatu mara baada ya mtambo namba 9 wenye uwezo wa kuzalisha megawati 235 kufanyiwa majaribio jana na mwingine utajaribiwa mwezi wa machi hali ambayo itaondoa adha ya umeme nchini

Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga

Kauli hiyo ameitoa hii leo Februari 16, 2024, bungeni jijini Dodoma baada ya kuulizwa swali na Spika wa Bunge Dkt Tulia Ackson kwamba ni lini mgao wa umeme utamalizika katika Taifa hili

"Tuliahidi mwezi huu tuna ratiba ya kuzindua mtambo huu (mtambo no 9 katika mradi wa Bwawa la Julius Nyerere) na ratiba hii iko palepale, tunawashukuru sana Watanzania kwa kuendelea kutuvumilia, matumizi ya umeme yanategemeana tukizalisha mwezi huu mgao utakuwa umepungua kwa kiasi kikubwa kwa sababu tunazalisha megawati 235 na mwezi wa tatu tutazalisha megawati 235 hivyo zitakuwa megawati 470 uhakika ni kwamba kufikia mwezi wa tatu mgao wa umeme utaisha nchini," amesema Naibu Waziri Kapinga

Kufuatia kauli hiyo Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, akaipa serikali muda na kuitaka ifikapo Juni mwaka huu tatizo la mgao wa umeme libaki kuwa historia nchini.