Friday , 22nd Dec , 2023

Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limesema kuwa kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama linaendelea kuimarisha ulinzi kuelekea sikukuu za krismasi na mwaka mpya litahakikisha sikukuu hizo zinasherekewa kwa amani na utulivu hasa ikizingatiwa kuwa mkoa huo ni kitovu cha utalii.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Justine Masejo

Akitoa taarifa hiyo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Justine Masejo, amesema katika kuhakikisha sikukuu hizo zinasherehekewa kwa amani na utulivu Jeshi hilo litahakikisha linatoa ulinzi kwenye nyumba za ibada, kumbi za starehe pamoja na maeneo mengine yote ambapo Askari watapangwa katika doria za miguu, pikipiki, magari na doria za mbwa.

Kamanda Masejo amewataka wazazi kuacha kuwapeleka watoto kwenye kumbi za starehe maarufu (disco toto), pia amepiga marufuku kwa madereva kuendesha magari wakiwa wamelewa, huku akiwata wamiliki wa bar wazingatie masharti ya leseni zao ambazo zinaonyesha muda halisi wa kufunga, halikadhalika kwa wamiliki wa kumbi na maeneo mengine ya starehe wanapaswa kuzingatia usalama katika maeneo yao na kutojaza watu kupita kiasi.