Saturday , 16th Dec , 2023

Waziri wa Madini Mh. Anthony Mavunde amesema Mfuko wa Dhamana  ya Mikopo unaosimamiwa na Wizara ya Fedha umelenga kusimamia upatikanaji wa mitaji kwa wachimbaji,wachenjuaji na wafanyabiashara wa madini kwa lengo la kuongeza uzalishaji na kusaidia upatikanaji wa fedha za Kigeni

Waziri Mavunde ameyasema hayo jana Jijini Dodoma wakati wa mkutano wa pamoja kati ya Wizara ya Madini,Fedha,Benki Kuu ya Tanzania(BOT) na wadau wa sekta ya madini kujadili namna ya uwezeshwaji mitaji kwa wachimbaji,wachenjuaji na wafanyabiashara wa madini.

“Ninafahamu kwamba asilimia kubwa ya wadau mna changamoto ya fedha za mitaji na uendeshaji wa shughuli zenu na hivyo kupelekea kupokea fedha hizo kwa wanunuzi wa madini waliopo nje ya nchi.

Ni maelekezo ya Mh Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwajengea uwezo watanzania kushiriki kikamilifu katika uchumi huu wa madini.

Hivyo kupitia Mfuko wa Dhamana ya Mikopo(Credit Guarantee Scheme) tutasimamia kuona wadau wa sekta ya madini wananufaika kwa kupata mitaji kupitia benki za biashara ili kuchochea uzalishaji na upatikanaji wa madini ambao utasaidia kukuza uchumi wa Taifa na upatikanaji wa fedha za kigeni”Alisema Mavunde

Akitoa maelezo ya awali Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Ndg. Msafiri Mbibo amesema lengo la mkutano huo ni majadiliano ya pamoja kati ya serikali na wadau wa madini kuona namna bora ya uwezeshwaji wa fedha za mtaji ili kuchochea uzalishaji wa madini na kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi.

Naye Mkurugenzi wa Masoko ya Fedha wa Benki Kuu Tanzania(BOT) Ndg . Emmanuel Akaro amesema kwamba Benki Kuu ya Tanzania itaendelea na zoezi lake la kununua dhahabu kutoka kwa wadau na kwamba kwa mwaka huu wa fedha wamejipanga kununua kuanzia tani 6,hivyo kwa kujengewa uwezo wa kimtaji kwa wafanyabishara wa madini wa ndani kutasaidia pia upatikanaji kwa urahisi wa soko la dhahabu ambalo BOT imekuwa mmoja wa wanunuzi wakubwa.