Thursday , 14th Dec , 2023

Waziri wa Mambo ya Nje January Makamba amesema kuwa kijana wa Kitanzania Joshua Mollel aliyekuwa anasoma nchini Israel, ambaye alikuwa akitafutwa tangu Oktoba 7, 2023 mara baada ya wanamgambo wa Hamas kuishambulia Israel, imebainika kwamba aliuawa mara baada ya kutekwa na wanamgambo hao.

Waziri wa Mambo ya Nje January Makamba

Waziri Makamba ameyabainisha hayo leo Desemba 14, 2023, kupitia ukurasa wake wa X na kusema taarifa hizo amezipata kutoka kwenye serikali ya Israel

"Nimeongea na Mzee Mollel, baba mzazi wa Joshua, kuhusu ujumbe huo wa serikali ya Israel, tunaendelea na mpango wa awali wa kuwapeleka Mzee Mollel na mwanafamilia mwingine pamoja na Afisa wa Serikali nchini Israel, kuungana na Balozi wetu na maafisa waliopo huko, kukutana na kuzungumza na mamlaka za nchi hiyo ili kupata taarifa za ziada, kwa ridhaa ya familia, na itakapobidi, tutatoa taarifa za ziada katika siku zijazo," imeeleza taarifa ya Waziri Makamba.

Huyu anakuwa ni Mtanzania wa pili kupoteza maisha kutokana na mapigano hayo kati ya wanamgambo wa Hamas na Taifa la Israel, ambapo Novemba 17 mwaka huu serikali ilitangaza kifo cha Clemence Felix Mtenga ambao ulirejeshwa nchini na kuzikwa, ambapo licha ya kutangaza kifo hicho lakini haikuwekwa wazi ni kipi hasa chanzo cha Mtanzania huyo kupoteza maisha 

Ikumbukwe hao miongoni mwa vijana wa Kitanzania wapatao 260 waliokwenda nchini Israel kushiriki mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa vitendo chini ya Mpango wa Ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Israel.