Friday , 3rd Nov , 2023

Mbunge wa Tarime vijijini, Mwita Waitara,amependekeza hatua mbalimbali kuchukuliwa ikiwemo kunyongwa kwa wale wote watakaothibitika kuhusika na upigaji wa fedha za umma.

Mbunge wa Tarime vijijini, Mwita Waitara

Mbunge Waitara amesema hayo bungeni jijini Dodoma leo Novemba 3, 2023 wakati akichangia taarifa za Kamati za bunge kuhusu ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

"Mimi nina mapendekezo yasiyo laini sana, ningependekeza wale wote ambao imethibitika bila shaka kwamba wamekula fedha za Watanzania, Mhe. Rais tumsaidie na wabunge tufanya maamuzi, wale wote walioiba bila kuwaonea kwenye nchi hii wanyongwe watoke tubaki na watu wema, wale walioonekana ni wazembe na wana nafasi katika umma hawa wafukuzwe kazi wakae mtaani," amesema Mbunge Waitara

Mapendekezo ya Mbunge Waitara kwa wezi wa fedha za umma kunyongwa yameungwa mkono na Mbunge Mbogwe Nicodemus Maganga ambaye amewaomba wabunge kutunga na kupitisha sheria hiyo itakayoruhusu wezi wa fedha za umma kunyongwa ili kumaliza tatizo hilo.