Friday , 8th Sep , 2023

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa ameielekeza Wizara ya Kilimo kusimamia kwa ukamilifu zoezi la ugawaji wa mbolea kwa wakulima ikiwemo kuongeza vituo vya mauzo na kuboresha mifumo ya upatikanaji wa mbolea kwa wakulima.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa maelekezo hayo leo Septemba 08, 2023 bungeni jijini Dodoma ambapo amesema serikali itaendelea kutoa ruzuku ya mbolea kwa wakulima ili kuwapunguzia makali ya bei ya pembejeo hiyo muhimu katika uzalishaji wa mazao ya kilimo.

"Katika msimu huu wa kilimo 2022/2023 matumizi ya mbolea yaliongezeka kutoka tani 363,599 hadi tani 538,000 sawa na ongezeko la 48%, ongezeko hili limetokana na upatikanaji wa mbolea ya ruzuku ambayo serikali imekuwa ikitoa kuanzia msimu wa kilimo 2022/2023" alisema Mhe. Kassim Majaliwa.

Aidha Waziri Mkuu amesema ongezeko la matumizi ya mbolea limeenda sambamba na ongezeko la uzalishaji hususani mazao ya chakula ambapo upatikanaji wa chakula sasa umeongezeka hapa nchini. 

"Matarajio ya mahitaji ya mbolea nchini kwa msimu wa kilimo 2023/24 ni tan 849,219 hadi kufikia tarehe 31 mwezi wa nane upatikanaji wa mbolea umefikia tani 480,622 sawa na asilimia 52.6 ya wastani wa mahitaji ya mwaka" alisema Waziri Mkuu, Mhe. Majaliwa.

Katika kuhakikisha mazao yaliyovunwa msimu wa 2022-23 yanapata soko, Waziri Mkuu amesema serikali kupitia wakala wa uhifadhi wa chakula NFRA imepanga kununua tani 305,000 za nafaka, hadi kufikia tarehe 5 septemba jumla ya tani 175,000 za nafaka sawa na asilimia 57 za lengo zimeshanunuliwa kupitia katika vituo vilivyopo katika kanda nane vya NFRA

Katika msimu 2022/23 bei za mazao mengine zimeendelea kuimarika hususani mazao yanayotumia mfumo wa stakabadhi ghalani mathalani zao la kakao linalolimwa kwa wingi wilaya ya Kyelwa na mvomero bei imefikia 8700 kwa kilo ukilinganisha na bei ya awali ya 2500

Kwa upande wa zao la Mbaazi bei imeongezeka kutoka shilingi 1500 kwa kilo hadi 2100 kwa kilo katika mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi lakini pia mkoa wa Manyara, bei ya Ufuta imeongezeka na kufikia 4000 kwa kilo ikilinganishwa na bei ya awali ya shiling 1000 hadi 1200 kwa kilo. 

Waziri Mkuu Majaliwa pia ametoa wito kwa wakulima kuendelea kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani kwa mazao haya kwa sababu imeonekana kuwa tija ya bei nzuri inayopatikana.

"Hivi karibuni kulionekana video kutoka wilaya ya Nanyumbu wakicheza ngoma kusherehekea kupatikana bei nzuri ya zao hilo" Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.