
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe, alibainisha hayo kwa niaba ya Waziri wa Fedha, wakati akijibu swali bungeni jijini Dodoma la Mbunge wa Baraza la Wawakilishi, Mhe. Ameir Abdalla Ameir, aliyetaka kujua idadi ya wafanyabiashara ambao hawajaingizwa katika mfumo rasmi wa kodi na Serikali inachukua hatua gani kuwafikia.
Mhe. Kigahe alisema kuwa, Serikali inatenga na kujenga maeneo maalumu ya masoko kwa wafanyabiashara wadogo na kuendelea kutoa elimu na ufafanuzi wa kina kwa wananchi kuhusu masuala ya kodi ili kuhamasisha wananchi kurasimisha biashara na shughuli za kiuchumi kwa hiari.
Alisema kuwa hadi Juni 30, 2023 Mamlaka ya Mapato Tanzania ilikuwa imesajili jumla ya walipa kodi takribani milioni 4.7 sawa na asilimia 16 ya idadi ya nguvu kazi iliyopo nchini ambayo ni takribani watu milioni 33.
Alieleza kuwa idadi ndogo ya usajili wa walipakodi, ikilinganishwa na fursa ya nguvu kazi iliyopo inatokana na sehemu kubwa ya shughuli za kiuchumi hapa nchini kuendeshwa na sekta isiyo rasmi inayokadiriwa kuajiri takribrani watu milioni 27.7.