Tuesday , 29th Aug , 2023

Serikali imesema kuwa inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kulinda thamani ya shilingi ya Tanzania ikiwemo kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na kuvutia uwekezaji kutoka nje.

Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba

Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, wakati akijibu swali la Mbunge wa Mbogwe, Nicodemas Maganga, aliyetaka kujua mikakati ya serikali kuongeza thamani ya shilingi ya Tanzania ikilinganishwa na nchi jirani za Afrika Mashariki.

Waziri Nchemba amesema serikali inaendelea kulinda thamani ya shilingi nchini ikiwa ni pamoja na kushughulikia tatizo la upungufu wa dola ili kuweza kukabiliana na changamoto inayoendelea kutokea duniani.

Amesema miongoni mwa hatua zinachukuliwa na Serikali ni pamoja na kushirikisha sekta binafsi katika kuimarisha mikakati ya kuongeza mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi pamoja na kuhimiza wananchi kuongeza matumizi ya bidhaa na huduma zinazozalishwa hapa nchini ili kupunguza mahitaji ya fedha za kigeni.

Alisema Serikali pia itaendelea kusimamia kwa karibu wazalishaji wa ndani ili kuongeza ubora katika uzalishaji wa bidhaa na huduma kwa lengo la kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi.

Pia serikali itaendelea kuongeza vyanzo vya upatikanaji wa fedha za kigeni ikiwemo ununuzi wa dhahabu na kusimamia utekelezaji wa sera ya fedha ili kuhakikisha utulivu wa mfumuko wa bei nchini.