Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega wakati akizungumza
Waziri Ulega ameyasema hayo wakati wa kikao cha kuwasilisha taarifa ya hali ya sekta ya mifugo nchini kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo kilichofanyika jijini Dodoma leo Agosti 24, 2023.
Amesema serikali ipo katika mpango wa kuweka miundombinu mizuri ikiwemo majosho na mabwawa ya kunyweshea mifugo itakayowawezesha wafugaji kufanya shughuli zao za unenepeshaji wa mifugo na kuivuna ili kukuza kipato chao.
Aliongeza kuwa wataweka utaratibu mzuri wa kuwapata vijana na wafugaji wengine ambao watakuwa tayari kupeleka mifugo yao katika gesti hizo lengo likiwa kuwafanya wafugaji waone tija ya ufugaji wa kisasa na kuondokana na ufugaji wa kuhamahama ambao umekuwa ukiwaingiza matatizoni kila uchao.
Alifafanua kuwa kwa kuanza wataweka miundombinu hiyo katika Ranchi ya Mkata iliyopo mkoani Morogoro ili kuwapa nafasi wafugaji waliopo katika Bonde la Mto Kilombero waweze kufanya ufugaji wao humo ili waondokane na ufugaji holela.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, David Kihenzile amesema kuwa mpango huo ni mzuri hivyo Wizara ifanye haraka uanze kuutekeleza kwa gharama nafuu huku akiongeza kuwa ni muhimu wizara kuona uwezekano mpango huo kuenea nchi nzima ili vijana na wafugaji wengine waweze kunufaika nao.