Wednesday , 9th Aug , 2023

Wananchi wa Kitongoji cha Ihula kilichopo Kata ya Gibishi Halmashauri ya wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu wameamua kujenga nyumba za tope ili kuwawezesha Walimu kuishi jirani na shule.

Nyumba za Walimu Ihula

Wananchi hao wamesema walimu wakiwa karibu na mazingira ya shule wanao uhakikia wa kuwahi hususani vipindi vya asubuhi hivyo kuwawezesha watoto wao kuanza kufundishwa mapema.

"Tumeamua tujenge nyumba ili watoto wetu wapate huduma ya kufundishwa, hatuna nguvu ya kuwajengea nyumba ya block ndio maana tukaamua tujenge nyumba ya tope ili wasogee huku," amesema Loli Machama ambaye ni mwananchi

Awali Mwenyekiti wa Kitongiji cha Ihula amesema waliamua kujenga nyumba hizo za muda huku wakiendelea na shughuli zingine za maendeleo kwenye kitongoji hicho.

"Hapa tumekaa tukaona tulipoletewa walimu tukaona tufanyaje tuwapangishie hata mwezi mmoja ili tuwajengee nyumba za muda,"" amesema Mwenyekiti

Nao baadhi ya walimu wa shule ya msingi Ihula wamepongeza uamuzi wa wananchi hao huku wakiomba serikali kuongeza nguvu katika ujenzi wa nyumba za kudumu.

"Sina muda mrefu nimefika shule hii, lakini maendeleo ninayoyaona ambayo yanatolewa na wanakijiji wa kijiji hichi sio mabaya kwasababu tunatengenezewa au tunajengewa nyumba za muda tunaziona, sio nzuri sana lakini kwa kipindi hicho kifupi zitatusaidia" Elinipahi Malima, Mwalimu shule ya msingi Ihula