
Wafanyabiashara hao wanamiliki makampuni yanayohusika na sekta za elimu, afya, kilimo, madini, mafuta na gesi, utalii, ujenzi, utafiti na ushauri wa kibiashara.
Ametoa pongezi hizo wakati akizungumza nao jijini St. Petersburg, Urusi ambako alimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano wa Pili wa Kilele baina ya Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka mataifa ya Afrika na Urusi.
“Udhahiri wa sekta binafsi umeonekana leo kwa kitendo chenu cha kushiriki Expo Forum na mimi nataka niwathibitishie kuwa mnao uwezo mkubwa wa kutafuta mitaji na rasilmali mbalimbali. Niwasihi muungane mkono ili muweze kuwafikia wazalishaji wakubwa huku mkiwaeleza kuwa Tanzania ni nchi iliyokaa kimkakati kwenye sekta ya kibiashara,” Amesema.
Mapema akisoma risala kwa niaba ya wenzake, Mwenyekiti wa wafanyabiashara hao Otieno Igogo amesema walikuja na bidhaa mbalimbali ili kuzitangaza na kutafuta fursa za kibiashara kwenye soko la Urusi. Miongoni mwazo ni korosho, mafuta ya alizeti, kahawa, rosella, viungo mbalimbali, mvinyo na zabibu.
Igogo amemweleza Waziri Mkuu kwamba makampuni 10 kati ya 19 yaliyoshirki kongamano hilo kutoka Tanzania yameweza kusaini mikataba ya ushirikiano wa kibishara na makampuni 11 toka Urusi ilhali makampuni mengine matano bado yako kwenye maongezi ya ushirika wa kibiashara.
Mkutano huo uilihudhuriwa na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Tabia Maulid Mwita, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Mbarouk, Naibu wa Waziri wa Fedha na Mipango wa Zanzibar, Ally Suleiman Ameir, Balozi wa Tanzania nchini Urusi, Balozi Fredrick Kibuta na watendaji wengine wa Serikali.