Monday , 10th Jul , 2023

Mgonjwa anayepatiwa matibabu katika Taasisi ya Mifupa (MOI), Dar es Salaam, jina lake limehifadhiwa, ambaye video yake imesambaa mitandaoni ikimuonesha yeye na mpenzi wake wakibusiana kwa ulimi ameomba radhi kwa kufanya kitendo hicho ambacho ni kinyume na maadili na kusema hatorudia tena.

Wakipigana mabusu

Kitendo cha wawili hao kubusiana wodini kimefanyika jana Julai 9, 2023, ambapo video hiyo ilirekodiwa na mmoja wa wagonjwa aliyekuwa katika kitanda cha jirani.

Aidha Taasisi hiyo imesema kwamba mpenzi wa mgonjwa huyo si mtumishi wa MOl.

"Menejimenti ya MOI inalaani kitendo hicho cha uvunjifu wa maadili kilichofanywa na mgonjwa huyo pamoja na mpenzi wake, vilevile Menejimenti inalaani na kukemea kitendo cha kurekodi video wodini na kutuma kwenye mitandao ya kijamii kilichofanywa na mgonjwa jirani, matukio haya yote ni kinyume na mwongozo wa Wizara ya Afya unaozuia kufanya matendo ya uvunjifu wa maadili kwa mgonjwa na kurekodi video wodini," imeeleza taarifa iliyotolewa na Mvungi ambaye ni Meneja Uhusiano MOI

Pamoja na hayo yote menejimenti inaendelea kuchunguza zaidi tukio hilo ili kujiridhisha kuwa hapakuwa na uzembe katika kusimamia usalama wa wagonjwa wakati ndugu wanawatembelea wagonjwa wodini.