Sunday , 2nd Jul , 2023

Ubalozi wa Tanzania nchini China umewataka Watanzania wanaosafiri kwenda katika Jiji la Hong Kong kukamilisha taratibu za safari zao, ikiwemo barua ya mwaliko kutoka kwa mwenyeji ili kuepuka usumbufu utakaojitokeza.

Hong Kong

Utaratibu huo umetolewa baada ya baadhi ya Watanzania wanaosafiri kwenda Hong Kong kuzuiwa kuingia au kuhojiwa kwa muda mrefu na maofisa wa idara ya uhamiaji katika uwanja wa ndege kutokana na matukio ya siku za nyuma ambapo baadhi ya watu waliokuwa na hati za kusafiria za Tanzania kufanya vitendo vya uvunjifu wa sheria.

Taarifa iliyotolewa leo Julai 2, 2023 na ubalozi huo imetaja taratibu nyingine ni pamoja na tiketi ya abiria itakayoonesha tarehe ya kuondoka Hong Kong na ‘booking’ ya hoteli inayoonesha jina la msafiri, tarehe ya kuingia na kutoka.

Hali hiyo imejitokeza zaidi katika kipindi cha hivi karibuni baada ya Hong Kong kufungua mipaka yake kuruhusu wageni kuingia ikiwa ni miaka mitatu ya zuio la eneo hilo ajili ya udhibiti wa maambukizi ya Uviko-19.

Katika taarifa hiyo, ubalozi wa Tanzania, umesema kutokana na kadhia hiyo Machi 30, 2023 uliwasiliana na mamlaka za Hong Kong kueleza kutoridhishwa na hatua inayochukuliwa na maofisa wa uhamiaji wa jiji hilo ya kutaka kila mwenye hati ya kusafiria ya Tanzania kuhojiwa kwa muda mrefu na wengine wachache kurejeshwa.