
Matamshi ya Emmanuel Macron yanajiri baada ya maandamano ya kupinga mauaji hayo yaliyolikumba eneo la Paris usiku wa kuamkia leo.Nahel, mwenye umri wa miaka 17, alipigwa risasi ndani ya gari lake baada ya kushindwa kusimama wakati alipoamriwa.
Video kwenye mitandao ya kijamii inamuonesha afisa mmoja akielekeza bunduki kwa dereva wa gari, kabla ya milio ya risasi kusikika na gari hilo kisha kuanguka na kusimama. Kijana huyo alifariki kutokana na majeraha ya risasi kifuani, licha ya msaada wa huduma za dharura.
Afisa huyo anayetuhumiwa kumpiga risasi amekamatwa kwa tuhuma za mauaji, huku video hiyo ikionekana kukanusha madai yake ya awali kwamba alifyatua risasi kwa sababu alihisi maisha yake yako hatarini.
Mfululizo wa maandamano ulifuatia shambulizi hilo la risasi usiku wa Jumanne huko Nanterre, eneo la magharibi mwa Paris ambako kijana huyo aliuawa. Watu 31 walikamatwa kufuatia ghasia hizo.