Tuesday , 9th May , 2023

Wizara ya Afya imesema ni kosa kisheria kwa duka lolote la dawa nchini kutoa huduma za kitabibu ikiwa ni pamoja na kuchoma sindano, kufanya tohara au vipimo vya maabara.

Esther Mkombozi , aliyepata madhara baada ya kuchoma sindano duka la dawa

Hatua hiyo imekuja kufuatia video moja kusambaa mitandaoni ikimuonesha Esther Mkombozi mkazi wa Arusha aliyeeleza kuwa alichomwa sindano katika duka la dawa na kumsababishia madhara katika mkono wake.

"Tunampa pole Esther kutokana na madhara aliyopata, tuwaombe wananchi kuendelea kuwa watulivu ambapo suala hill linafanyiwa kazi," imeeleza taarifa ya Wizara ya Afya

Kutokana na hilo, Wizara imeelekeza Baraza la Famasi (PC) na Bodi ya Hospitali Binafsi (PHAB) kufuatilia suala hilo mara moja na hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa wote watakaobainika kukiuka sheria, kanuni, miongozo na Taratibu za Usimamizi na Udhibiti wa utoaji wa huduma za Afya nchini.