Maandalizi yakiendelea bandarini
Rais wa Ujerumani Joachim Gauck ambaye anatarajiwa kufanya ziara ya siku moja kisiwani Zanzibar siku ya Jumatano anakuwa Rais wa kwanza kuwasili Zanzibar kwa kutumia usafiri wa baharini na kutotumia usafiri wa magari wakati wa mapokezi.
Kwa mujibu wa taarifa ya ikulu iliyotolewa mjini Zanzibar na kusambazwa kwa vyombo vya habari kupitia mkuu wa mkoa wa Mjini Magahribi Abdullah Mwinyi amesema kiongozi huyo atapokolewa bandarini Zanzibar na mwenyeji wake Dkt Ali Mohmaed Shein na kupigiwa mizinga 21 kwa heshima yake na badaye kuanza msafara wake kwa miguu huku akisalimia wananchi kuelekea hoteli ya Serena iliyoko umbali wa kilomita moja..
Aidha mkuu huyo wa mkoa amesema akiwepo hapa Zanzibar atapata fursa ya kuonana na viongozi wa dini na kufanya nao mazungumzo huku mke wake Bi Daniela Schadt akifungua shule ya maandalizi ya Herrn hunter Academy iliopo Mwera wilaya ya Magharibi.
Ujio wa kiongozi huyo kwa kutumia usafiri wa boti umesababisha barabara itakayotumika kuanza kukarabatiwa na usafi na ulinzi kuimarishwa bandarini huku utaratibi wa kuingia na kutoka bandarini ukiwa sio wa kawaida ..