Monday , 2nd Feb , 2015

Wafanyabiashara wa kati na wadogo zaidi ya 600 wenye maduka katika jiji la Mwanza wameazimia kufunga maduka yao kila mara kesi ya mwenyekiti wao itakapokuwa inatajwa mahakamani.

Siku chache baada ya mwenyekiti wa jumuiya ya wafanyabiashara Tanzania Johnson Minja kufikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi wilaya ya Dodoma akikabiliwa na kesi ya kudaiwa kushawishi wafanyabiashara kutenda kosa la jinai la kutolipa kodi na kudaiwa kuzuia ukusanyaji wa kodi kwa kutumia mashine za kodi za kielektroniki (EFD’s ), wafanyabiashara wa kati na wadogo zaidi ya 600 wenye maduka katika jiji la Mwanza wameazimia kufunga maduka yao kila mara kesi hiyo itakapokuwa inatajwa mahakamani.
 
Azimio hilo la pamoja limefikiwa katika kikao cha wafanyabiashara kilichoongozwa na mwenyekiti wa jumuiya ya wafanyabiashara mkoa wa Mwanza Christopher Wambura, siku nne baada ya maduka yao kufunguliwa na kuanza kutoa huduma kama kawaida.

Kesi hiyo itatajwa tena Februari 11 mwaka huu, siku ambayo wafanyabiashara wa maduka jijini Mwanza wamepanga kufunga maduka yao.

 
Wakati wafanyabiashara hao wakiweka msimamo wao wa kufunga maduka baadhi ya wafanyabiashara jijini Mwanza wanaotumia mpaka wa Sirari kuingiza bidhaa zao nchini wamewalalamikia baadhi ya watumishi wa mamlaka ya mapato Tanzania TRA kwa unyanyasaji.

Naye Meneja msaidizi wa mamlaka ya mapato tanzania (TRA), mkoa wa Mwanza anayeshughulikia forodha na ushuru Sebastian Kimaro amewataka wafanyabiashara wanaodai kunyanyaswa na kuombwa rushwa na baadhi ya watumishi wa TRA wasio waaminifu kutoa taarifa mara moja ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua kali za kinidhamu na kisheria.

Wafanyabiashara hao wamechangishana shilingi 30,000 kila mmoja ili ziweze kusaidia uendeshaji wa kesi inayomkabili mwenyekiti huyo wa jumuiya ya wafanyabiashara Tanzania,