Friday , 29th Jul , 2022

Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana amewataka wadau wa sekta ya  Misitu katika maeneo mbalimbali nchini kutumia mitambo na vifaa vinavyo tengenezwa nchini Tanzania kwa ajili ya shughuli za utayarishaji na uchakataji wa mazao ya Misitu

Amesema lengo ni kurahisisha upatikanaji wa bidhaa hizo hapa nchini na kuchangia  Pato la Taifa

Dkt. Pindi Chana amesema hayo Wilayani Mafinga wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua  shughuli za mafunzo na utengenezaji wa bidhaa zinazotokana na Mazao ya Misitu katika Kituo cha mradi wa Panda Miti Kibiashara (PFP2)

Waziri Balozi Dkt. Chana amesema, Tanzania imebarikiwa kuwa na tunu na amani inayoendelezwa na  kulindwa na Uongozi Bora wa Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania hali inayo wavutia wawekezaji wengi na kuongeza kuwa jitihada hizo ni lazima ziungwe mkono kwa kutumia bidhaa za hapa nchini.

Licha ya kuupongeza uongozi wa Mradi huo, Waziri Balozi Dkt. Pindi Chana amesema  Wizara anayoiongoza itaendelea kushirikiana na Sekta Binafsi hususan wawekezaji ili kuyapa thamani mazao ya Utalii, kupanua wigo wa ajira kwa wananchi, kuimarisha mahusiano ya Kimataifa pamoja na kuongeza Pato la Taifa. 

Akiwa kwenye eneo  hilo la mradi Balozi Dkt. Chana ameshuhudia  shughuli za uandaaji wa miche ya miti, mashine mbalimbali za kupasulia mbao, utengenezaji wa bidhaa zitokanazo na misitu kama vile mkaa, samani, mafunzo na maabara ya kutibu miti iliyo vunwa