Saturday , 19th Feb , 2022

Beki wa Simba, Shomary Kapombe amekiri penalti aliyopiga katika mchezo uliopita dhidi ya Asec Mimosas ni kama alijilipua tu kwa kujiamini kwa kuvaa ujasiri baada ya kubaini wenzake walikuwa na mchecheto kwenda kuipiga.

(Beki wa kulia wa SImba SC, Shomari Kapombe akimiliki mpira)

Kapombe alifunga penalti hiyo wakati Simba ikiishindilia Asec mabao 3-1 katika mechi ya kwanza ya kundi D ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya Yusuph Mhilu kuchezewa madhambi na kipa wa Asec, Karim Cisse.

“Kila siku baada ya mazoezi ya kawaida nimekuwa na muda wa kupiga penalti na hilo ndilo lilinipa ujasiri wa kwenda kubeba jukumu hilo ambalo lilikuwa gumu,” amesema Kapombe.

Mara baada ya mwamuzi Souleiman Djama kutoka Djibouti kuamuru adhabu hiyo ilionekana wachezaji wa Simba kama wakikwepa kwenda kupiga kabla ya Kapombe kuubeba mpira na kufunga kiufundi na kuifungia timu yake bao la pili na kushiriki kwenye ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Vinara wa Ligi kuu ya Ivory Coast, ASEC Mimosas.