Monday , 2nd Aug , 2021

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameimwagia sifa za pongezi timu ya taifa ya Tanzania ya vijana chini ya miaka ishirini na tatu baada ya vijana hao kuliwakilisha taifa vema kwa kuwa mabingwa wa michuano ya CECAFA kwa msimu huu 2021.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akitoa neno kwenye moja ya hotuba zake.

Tanzania U23 imeibuka na ubingwa huo baada ya kuifunga timu ya vijana ya Burundi kwa penalti 6-5 kufuatia sare ya bila kufungana ndani ya dakika tisini kwenye mchezo uliochezwa Jumanne ya  Julai 2, 2021 nchini Ethiopia na kuchukua Ubingwa huo kwa mara ya kwanza.

Rais Samia, amezituma salamu hizo za pongezi jioni ya jana Jumapili, Agosti 1, 2021kupitia akaunti yake ya Twitter baada ya mabingwa hao kuwasili nchini saa kumi na mbili na nusu asubuhi wakitokea nchini Ethiopia ambapo michuano hiyo ilipofanyika.

Salamu za pongezi za Rais Samia zinasomeka kuwa;

“Nawapongeza timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 23 kwa kutwaa ubingwa wa Mashindano ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA-2021). Ushindi huu ni heshima kwa nchi yetu na ni chachu ya kukuza michezo. Natoa wito kwa wadau wa michezo kuendeleza jitihada za kukuza michezo yetu”.