Monday , 28th Jun , 2021

Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya, leo Juni 28, 2021, imemuachia huru kada wa CHADEMA, Mdude Nyagali, baada ya kumkuta hana hatia katika kesi yake iliyokuwa ikimkabili ya kusafirisha madawa ya kulevya aina ya Heroin.

Kada wa CHADEMA Mdude Nyagali (wa pili kulia) alipokuwa Mahakamani

Mdude alifikishwa Mahakamani kwa mara ya kwanza Mei 13, 2020, baada ya Jeshi la polisi mkoa wa Mbeya kumkamata mnamo Mei 10 mwaka huo, katika msako uliofanyika maeneo ya Kadege stendi jijini humo, na baada ya kwenda nyumbani kwake na kufanya upekuzi walimkuta na unga uliodhaniwa kuwa ni dawa za kulevya aina ya Heroin Hydrochloride gramu 23. 4

Ambapo katika maelezo ya awali ya Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya Ulrich Matei, alisema kuwa dawa hizo za kulevya aina ya Heroin Hydrochloride, husababisha ulevi usioponyeka kirahisi na hatimaye hupelekea mtumiaji kuharibikiwa na akili na kwamba dawa hizo pia zimo kwenye kundi la kwanza la orodha za sumu.