Friday , 28th May , 2021

Kikosi cha wekundu wa Msimbazi Simba kimewasili salama mkoani Mtwara asubuhi ya leo Mei 28, 2021 kikitokea jijini Dar es Salaam ikiwa ni safari ya kuwafuta Namungo kuelekea mchezo wake wa kesho wa ligi kuu bara utakaochezwa saa 10:00 jioni kwenye dimba la Majaliwa.

Mshambuliaji wa klabu ya Simba, Meddie Kagere akiwasili na timu mkoani Mtwara asubuhi ya leo.

Baada ya Simba kuwasili mkoani Mtwara, wanategemea kusafiri tena kwa gari kuelekea mkoani Lindi ambapo ndio maskani ya Wauaji hao wa kusini, klabu ya Namungo ili kucheza mchezo wa kiporo cha mzunguko wa kwanza wa ligi kuu bara.

Simba ilishindwa kucheza mchezo huo kutokana na kuwa na majukumu ya kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya klabu bingwa barani Afrika ambapo waliondoshwa kwenye hatua ya robo fainali na Kaizer Chiefs ya Afrika ya kusini kwa kufungwa jumla ya mabao 4-3.

Kwa upande mwingine, Namungo alishindwa kucheza mchezo huo kutokana na sababu inayofanana na ya Simba lakini utofauti ukiwa, Namungo alikuwa anashiriki kombe la Shirikisho Afrika na kutolewa hatua ya Makundi na vilabu vya Raja Casablanca na Pyramids.

Ukigeukia upande wa takwimu, 

Simba anatakwimu nzuri kwani wamekutana na Namungo mara tatu na kufanikiwa kushinda michezo miwili na sare mara moja. Kwenye michezo miwili ya Ligi, Simba imeshinda mara moja na kutoka suluhu huku wakifungwa 2-1 kwenye kombe la Mapimduzi Januari 11, 2021.

Hivi sasa, Simba ipo nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa VPL wakiwa na alama 61 kwenye michezo 25 ilhali Namungo ipo nafasi ya 8 wakiwa na michezo 28 na alama 40.