Wednesday , 26th May , 2021

Mabingwa watetezi wa kombe la ligi ya kikapu nchini Marekani 'NBA', Los Angeles Lakers imeibuka na ushindi wa kwanza kwenye mchezo wa mzunguko wa pili wa hatua ya mtoano ya robo fainali ya ligi hiyo iliyochezwa usiku wa kuamkia leo dhidi ya Phoeniz Suns.

Nyota wa LA Lakers, Anthony David akijiandaa kuucheza mpira kwa Lebron James kwenye mchezo dhidi ya Phoenix Suns alfajiri ya kuamkia leo kwenye NBA Playoff

Lakers wamepata ushindi wa alama 109 kwa 102 na kuwafanya wawe na ushindi mmoja sawa na Phoenix Suns hivyo kuzidi kunogesha michezo hiyo mikubwa ya mtoano kuwa  na mvuti kwani wamesaliwa na michezo mitano kila mmoja akisaka ushindi wa michezo mitatu ili kusonga mbele.

Kwenye mchezo huo uliokuwa wakukata na shoka, nyota wawili wa Lakers, Lebron James na Anthony Davis ndiyo walioonesha utofauti mkubwa wa ubora mbele ya Suns, kwani Davis ameibuka kuwa nyota wa mchezo kwa kupata alama 234rebaundi 10 na assisti 7.

Lebron James amepata alama 23, rebaundi 4 na assisti 9 huku nyota wa Suns David Booker akiwa kinara kwa upande wa timu yake kwa kufikisha alama 31, rebaundi 1 na Assisti 3.

Kwa upande mwingine, Brooklyn Nets imezidi kujiweka kwenye mazingira mazuri baada ya kuibuka na ushindi wa alama 130 kwa 108 dhidi ya Boston Celtics na kupata ushindi wake wa pili mfululizo hivyo kusaka ushindi kwenye michezo miwili kati ya mitano iliyosalia ili kusonga mbele.

Nyota watatu wakali la Brooklyn Nets walioonesha kiwango kizuri ni pamoja na Kevin Durrant aliyeibuka kuwa nyota wa mchezo kwa kufikisha alama 26, 8 rebaundi na 5 assisti wakati James Harden akipata alama 20, rebaundi 5 na Assisti 7.

Irving alikusanya alama 15, rebaundi 6 na Assisti 6 na kumuacha hoi nyota wa Boston Celtics, Jason Tatum ambaye hakuwa na mchezo mzuri akikusanya alama 9, rebaundi 4 na Assisti 1.

Mchezo mwingine ulichezwa alfajiri ya kuamkia leo ni ule uliomalizika kwa Dallas Mavericks kwa alama 127 kwa 121 dhidi ya Los Angeles Clippers na kuwafunga kwenye mchezo wa mzunguko wa pili wa michezo ya mtoano ya NBA.

Kawhi Leonard wa Clippers ndiye aliyeibuka nyota wa mchezo licha ya timu yake kufungwa kwa kujikusanyia alama 41, rebaundi 6 na assisti 4 huku Paul Gerge akivuna alama 28, rebaundi 12 na assisti 6 na kumpiku Luka Doncic wa Dallas aliyepata alama 39, rebaundi 7 na assisti 7.

Michezo ya NBA Playoff itaendelea tena usiku wa kuamkia kesho kwa michezo mitatu, Philadelphia 76ers watakipiga na Washington Wizard saa 8:00 usiku, New York Knicks watacheza na Atalanta Hawks saa 8:30 usiku ilhali Utah Jazz watacheza na Memphis Glizzlies saa 11 Alfajiri.