Wednesday , 28th Apr , 2021

Waziri wa TAMISEMI Ummy Mwalimu, amemtaja mkuu wa mkoa wa Tanga Martine Shigella, kama mkuu wa mkoa bora kwani amekuwa akiwashirikisha katika masuala mbalimbali na kuwataka wakuu wengine wa mikoa kujitafakari na waige mfano bora kutoka kwake.

Kushoto ni mkuu wa mkoa wa Tanga Martine Shigella na kulia ni Waziri wa TAMISEMI Ummy Mwalimu

Waziri Ummy ameyasema hayo na kuelekeza kwamba serikali haitaweza kumvumilia kiongozi yeyote wa wilaya au mkoa ambaye hatokuwa na uwezo wa kushirikisha na kushirikiana na wenzake.

"Wakuu wa mikoa mingine wanatakiwa kujitafakari sababu hata tukikaa Bungeni tunawashangaa wabunge wenzetu wanavyogombana na wakuu wao wa mikoa, tunawaambia mbona sisi Tanga tupo vizuri na mkuu wetu wa mkoa? tena anatusemea, anatushirikisha na tunapanga naye", amesema Waziri Ummy

Aidha ameongeza kuwa, "Tanga tuna mkuu wa mkoa mzuri ambaye tunafanya kazi kama timu moja, hivyo wakuu wa mikoa wajue ukishakua kwenye nafasi hiyo maana yake ni kuwashirikisha wenzako na kushirikiana nao, kuwaongoza na kuwarekebisha wenzako"