Kikosi cha timu ya soka ya makipa wanaoshiriki ligi mbalimbali nchini
Timu ya soka ya umoja wa walinda mlango ama magolikipa wa timu zinazoshiriki ligi mbalimbali za soka hapa nchini Tanzania hii leo wamefanikiwa kutoka kimasomaso mara baada ya kuifunga timu ya Lugalo Veterani inayoundwa na nyota wa zamani waliowahi kutamba katika soka hapa nchini kwa bao 3-2 katika mchezo mkali uliopigwa katika viwanja vya jeshi lugalo jijini Dar es salaam
Akizungumza na muhtasari wa michezo mmoja wa waratibu wa timu ya magolikipa ambaye ni nahodha msaidizi wa timu hiyo Ivo Mapunda amesema lengo la kuunda timu hiyo ni kuanzisha taasisi au umoja wa magolikipa wote hapa nchini ili kuinua viwango vyao na pia kuibua makipa wapya hii ni kutokana na kuwepo kwa uhaba wa makipa hapa nchini
Mapunda ambaye ni golikipa namba moja kwa sasa katika klabu ya Simba amesema lengo lingine kuu ni kuibua makipa wapya na chipukizi ambao watarithi nafasi zao mara baada ya makipa ambao wanatamba sasa akiwemo yeye, Kaseja, Kado na wengine kutundika grove zao na hivyo inakuwa fursa sasa kwa vijana hao nao kuonesha uwezo wao nakusaidia timu za taifa
Aidha Mapunda amesema pamoja na soka lakini pia taasisi hiyo ya magolikipa itakuwa ikitoa huduma za jamii hasa kusaidia watu wasiojiweza na pia kutoa elimu hasa kwa vijana na wanamichezo juu ya athari za matumizi ya madawa ya kulevya na magonjwa hasa UKIMWI na mengineyo
Naye Nahodha wa timu hiyo Shaban Hassan Kado ameiambia muhtasari wa michezo kuwa timu hiyo ina faida kubwa sana kwa magolikipa kupata uzoefu wa kucheza kwa miguu na kupata pumzi ya kutosha hasa ikizingatiwa katika ligi muda mwingi wao hutumia mikono na hivyo wengi wao hukosa uzoefu wa kucheza na miguu
Aidha Kado ambaye ni kipa namba moja wa Wagosi wa Kaya Coastal Union ya Tanga ameongeza kusema kuwa jambo kubwa lingine la taasisi yao pamoja na kukuza na kuvumbua vipaji vya makipa pia ni kuleta umoja na kushirikiana na kuondoa dhana ya kuwa magolikipa wengi hasa wa ligi kuu kuwa hawapendani
Kwa upande wake nahodha wa timu ya Lugalo Veterani Benard Mgona Kifaru ameiambia muhtasari wa michezo kuwa uamuzi wa magolikipa kuwa na timu hiyo ni faida kwao hasa kipindi hiki ligi zimesimama kwakuwa wachezaji watakuwa wakijiweka fiti kimazoezi
Naye kocha mkuu wa Lugalo Veterani Tata Daniel Mwakatwila amekubali uwezo wa magolikipa hao na kusema wameonesha uwezo mkubwa na wanaweza kucheza ligi yoyote wakicheza nafasi za ndani tofauti na walizozoea