Saturday , 7th Nov , 2020

Maduka manne yameteketea kwa moto usiku wa kuamkia leo Novemba 7, 2020, katika soko maarufu la Kariakoo, lililopo mamlaka ya mji mdogo wa Katoro mkoani Geita, ambapo mpaka sasa chanzo cha moto huo bado hakijajulikana.

Maduka yaliyoteketea kwa moto

Akizungumza na EATV Kamanda wa Polisi mkoa wa Geita Henry Mwaibambe, amesema kuwa mpaka sasa wanaendelea kuimarisha ulinzi katika maeneo hayo ili kuepusha upotevu wa mali nyingine katika soko hilo.

"Tulipata taarifa ya kuzuka moto kwamba maduka manne yameathirika na kupitia jitihada za wananchi na Jeshi la Zimamoto wakafanikiwa kuuzima moto huo, lakini pia walijitahidi kuimarisha ulinzi ili wale watu waliotaka kutumia fursa hiyo kufanya uhalifu wasifanikiwe", amesema Kamanda Mwaibambe.

Kwa upande wao baadhi ya wahanga wa ajali hiyo wameiomba serikali kuhakikisha inaboresha miundombinu ya magari ya zimamoto ili kuweza kuokoa mali na vitu pale majanga yanapotokea.