
Meneja wa Klabu ya Simba, Patrick Rweyemamu (Pichani) akizungumza na Waandishi wa Habari .
"Tunaendelea kupokea ripoti za vyama husika za nchi ambazo wachezaji wanapotoka, ambapo sasa ni takribani wachezaji watano hadi sita, kuhusu majina yao watafahamishwa lakini asilimia 90 hadi 80 ya wachezaji tulionao wanahudumu katika timu zao za taiafa" amesema Rweyemamu.
Aidha, katika maandalizi ya kuelekea mchezo wa VPL siku ya Jumamosi dhidi ya Gwambina FC ya jijini Mwanza katika uwanja wa Benjamin Mkapa Dar Es Salaam meneja huyo amesema timu kwa sasa ipo kwenye mazoezi kujiandaa na mchezo huo
"Tuna wachezaji 28 tuliowasajili ni mchezaji mmoja tu ambaye ni Fraga peke yake atakayeukosa mchezo ujao kutokana na majeruhi lakini sipo tayari kuelezea ameumia kwa kiasi gani kwakuwa ni suala la kitabibu, taarifa za kitabibu zikitoka tutawafahamisha" amesema Rweyemamu
Gerson Fraga 'mkata umeme' kama anavyopendwa kuitwa na wapenzi wa Simba SC alitoka mapema katika mchezo wa Jumapili iliyopita dhidi ya Biashara United ya Mara katika uwanja wa Benjamin Mkapa na dakika 90 zikaisha kwa Simba kujinyakulia alama tatu kwa ushindi wa 4-0.
Fraga amekuwa na msimu mzuri 2019-20 kulinganisha na wachezaji wenzie wengine waliosajiliwa kikosini humo Tairone Santos na Wilker da Silver walioshindwa kufanya vizuri na kikosi hicho hivyo waliachwa katika usajili wa msimu mpya.
Kuhusu mchezo ujao dhidi ya Gwambina FC Rweyemamu amewataka washabiki na wapenzi wa timu hiyo wafike kwa wingi uwanjani kwani wao ni wachezaji wa 12 hivyo nafasi yao ni muhimu katika kuhakikisha kikosi chao kinafanya vizuri katika VPL msimu 2020-21