Wachezaji wa Bayern Munich wakipongezana baada ya kufunga bao kwenye moja ya michezo ya ligi ya mabingwa.
Kocha wa Bayern Hansi Flick amewataka wachezaji wake kusahau ushindi wa mabao 8-2 walioupata kwenye mchezo uliopita wa robo fainali dhidi ya Barcelona watakapo wavaa Lyon usiku wa leo.
Katika hatua ya 16 bora Lyon iliitoa Juventus na ikaifunga Manchester City mabao 3-1 katika mchezo wa hatua ya robo fainali, hiyo kocha wa Bayern anaelewa hatari walionayo Lyon katika mchezo wa leo.
Rudi Garcia kocha wa Olympique Lyon anasema anajua kuwa Bayern ni timu hatari lakini rekodi hazina nafasi katika mchezo wa leo. Katika michezo tisa ya michuano hii msimu huu the Bavarians wamefunga mabao 39 huku wao wakiruhsu mabao 8 tu.
Kocha Garcia anasema Man City walifunga zaidi ya mabao 100 kwenye ligi kuu England EPL, anasema kama tunaangalia takwimu basi hawana budi kubaki hotelini na kuwaachana Bayern wacheze peke yao. Hatupewi nafasi lakini tumezitoa timu kubwa mpaka kufika hapa amesema Garcia
Bayern Munich na Lyon wanakutana kwa mara ya tisa kwenye michuano ya vilabu barani ulaya. Bayern wameshinda mara 4 na Lyon wameshinda mara 2 huku wakitoka sare mara mbili. Mara ya mwisho kukutana katika michuano hii ilikuwa katika hataua ya nusu fainali ambapo Bayern walipata ushindi wa jumla wa mabao 4-0 msimu wa 2009-10.
Hii ni mara ya 12 Bayern wanacheza katika hatua ya nusu fainali ya michuano hii, ni Real Madrid pekee ndio iliyocheza nusu fainali nyingi zaidi ya the Bavarians wao wamecheza mara 13.
Kocha Rudi Garcia anaweza kuwa kocha wa pili raia wa ufaransa kuipeleka timu katika hatua ya Fainali ya klabu bingwa ulaya endapo kama ataifunga Bayern Munich. Kocha pekee aliyewahi kufanya hivyo ni Didier Deschamps akiwa na kikosi cha Monaco Msimu wa 2003-03.
Kwenye michuano yote barani ulaya Bayern ndio timu iliyocheza michezo mingi mfululizo pasipo kupoteza. Wamecheza michezo 28 katika michuano yote wameshinda michezo 27 na wametoka sare mchezo mmoja.
Vikosi vinavyoweza kuanza katika mchezo huu kwa timu zote mbili.
Lyon: Lopes; Denayer, Marcelo, Marçal; Dubois, Caqueret, Guimarães, Aouar, Cornet; Depay, Dembélé
Bayern: Neuer; Kimmich, Boateng, Alaba, Davies; Goretzka, Thiago; Perišić, Müller, Gnabry; Lewandowski