Monday , 27th Oct , 2014

Viongozi wa vyama vinavyounda UKAWA (CHADEMA, CUF, NCCR Mageuzi na NLD) wamesaini makubaliano ya kushirikiana katika chaguzi zote.

Vyama vya vinne vya siasa vya upinzania vinavyounda umoja wa katiba ya wananchi-Ukawa- vimesaini hati ya makubaliano ya ushirikiano ya kufanya kazi pamoja katika chaguzi mbalimbali ikiwemo uchaguzi mkuu wa Rais na Wabunge unaotarajiwa kufanyika mapema mwakani.

Akisoma makubaliano hayo kwa niaba ya makatibu wa kuu wa vyama hivyo, katibu mkuu wa CHADEMA Dkt Wilbrod Slaa amesema chini ya makubaliano hayo vyama hivyo vimekubaliana kuuwisha sera za vyama hivyo kwa kuchukua yale yanayofanana ili kuwa na kauli zinazofanana wanapozungumza na wananchi, pamoja na kushirikiana katika mchakato wa kuelimisha wananchi kupiga kura ya hapa kwa katiba mpya inayopendekezwa.

Wakizungumza baada ya kusaini hati ya makubaliano, mwenyekiti wa chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA amewatoa wito kwa viongzoi wa chama hicho katika mikoa kutokwamisha mipango ya UKAWA kwa kuwa ni mpango wa Mungu na kuwataka viongozi wa vyama vinavyounda umoja huo kuhacha kukaa maofisini kwenda kwa wananchi kuendeleza mapambano, huku mwenyekiti wa CUF taifa Prof Ibrahim Lipumba amewataka wananchi kutopiga kura ya ndiyo kwa Katiba Inayopendekezwa ili kuwezesha rasimali za nchi zitumike kwa faida ya wananchi wote.

Aidha kwa upande wao mwenyekiti wa chama cha NCCR- Mageuzi mhandisi James Mbatia amewataka viongozi wa vyama hivyo katika mikoa kukaa kuangalia wagombea wanaokubalika bila ya kujali chama na kuacha kulalamika ili kuwasaidia watanzania kupata maendeleo kupitia rasilimali zao, huku mwenyekiti wa chama cha NLD Dkt Emmanule Makaidi akisisitiza umuhimu wa kujenga umoja utakaosadia kuleta mageuzi yatakayoleta mchango mkubwa kiuchumi.

Makubaliano yamefanyika katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam na kushuhudiwa na maelfu ya wanachama, wapenzi na mashabiki wa vyama hivyo walikuwa wamebeba mabango yenye ujumbe mbalimbali ambao wengi wao wameingia kwa maandamano kutoka katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam.

Tags: