Aliyekua Rais wa awamu ya tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Benjamin William Mkapa enzi za uhai wake.
Akizungumza na East Africa Radio, Makamu Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Fredrick Mwakalebela amesema kuwa wamempoteza mwanachama na mshauri wao mkuu ambaye alikua akiwasaidia katika masuala mengi ambayo yalikua yanaihusu timu kipindi cha migogoro na hata ya mafanikio.
Mwakalebela ameongeza kuwa ndiye aliyeibua wazo la ujenzi wa Uwanja wa Taifa ambao umetoa fursa kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa michuano ya mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri wa miaka 17 ambayo ilipigwa hapa nchini mwaka 2019.
Hayati Mkapa aliwahi kuinusuru Yanga kupitia mgogoro ulioibuka miaka mingi iliyopita kati ya makundi mawili ya Yanga asili na Yanga kampuni ,ambapo aliwaita pande zote mbili kujadiliana kwa pamoja na kutuliza vuguvugu hilo lililotaka kuigawa klabu hiyo yenye maskani yake mitaa ya Twiga na Jangwani.
Uongozi huo wa Yanga umetoa pole kwa familia pamoja na ndugu jamaa na marafiki pia kwa Taifa kwa ujumla kwa kumpoteza mtu muhimu.








