Bondia Mfaume Mfaume akijifua kuelekea pambano lake na Arnel Tinampay Agosti 28
Bondia Mfaume Mfaume ameendelea na mazoezi kwa ajili ya kujiweka imara kuelekea pambano lake la kimataifa dhidi ya Bondia kutoka nchin Ufilipino, Arnel Tinampay, litakalofanyika mwezi ujao.
Ikiwa imebaki mwezi mmoja baada ya kujifua kwa miezi kabla ya pambano lake dhidi ya Arnel Tinampay Agosti 28 kugombea ubingwa wa kimataifa wa Mabara IBA, Bondia Mfaume Mfaume amesema amejiandaa vizuri na hatowaangusha Watanzania na atahakikisha bondia huyo wa Ufilipino hafiki raundi nyingi.
'' Nitampiga Mfilipino nahakikisha hafiki raundi ya 5, na nitawaambia wamlete Manny Pacquiao''.
Mfaume amewaomba Watanzania na wadau wa mchezo wa ngumi na wadhamini mbalimbali kumuunga mkono ili kuipeperusha vyema bendera ya Taifa.
Endapo Mfaume atashinda pambano hilo dhidi ya Tinampay, atakuwa Mwafrika wa kwanza kutwaa mkanda wa Kimataifa wa Mabara IBA.





