Kocha wa AC Milan Stefano Pioli
Klabu ya soka ya AC Milan imetangaza Jumanne hii kwamba Kocha Stefano Pioli amesaini nyongeza ya mkataba wa miaka miwili kwenye kandarasi yake, kuendelea kubaki klabuni hapo hadi Juni 2022.
Milan ilikuwa kwenye mazungumzo ya kumtema, Pioli klabuni hapo na kumpa mikoba yake kocha Ralf Rangnick, lakini wakala wa Mjerumani huyo alitoa taarifa mapema wiki hii kuwa wameamua kwa pamoja na klabu kusitisha mpango huo.
Tangu Serie A irejee tena, Milan chini ya Pioli imekuwa na kiwango bora sana ya kupata matokeo ya ushindi.
Rossoneri wameshinda michezo saba kati ya michezo yao tisa ya ligi tangu irejee tena, wakitoka sare mechi mbili.
Pioli alijiunga na Milan Oktoba 2019 kama mbadala wa Marco Giampaolo aliyefutwa kazi, baada ya kupoteza mechi zake nne tu kati ya saba za mwanzo.
Baada ya kuanza kibarua chake vibaya kwa matokeo mabovu, hatimaye Pioli mwenye umri wa miaka 54 ameirejesha timu hiyo katika nafasi ya tano kwenye msimamo wa Serie A.





