Tuesday , 14th Apr , 2020

Wakati huu dunia ikikimbia kwa teknolojia kila siku, mambo yako hivyo hata katika sekta ya michezo. Shughuli za michezo zilivyokuwa zikiendeshwa miaka 10 au 20 ya nyuma siyo sawa na zinavyoendeshwa hii leo.

Makao Makuu ya klabu ya Ihefu

Moja ya klabu ambayo imeyapokea mabadiliko hayo na kutaka kuonesha mfano ni klabu ya soka ya Ihefu inayopatikana Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya.

Klabu hiyo inamilikiwa na kampuni ya Highland Estates inayojishughulisha na shughuli mbalimbali za uzalishaji na kutoa huduma ikiwemo kilimo, ujenzi wa majengo, uuzaji wa mashine, uuzaji wa viwanja na mashamba na usafirishaji.

Klabu hiyo inayoshiriki ligi daraja la kwanza, imejizatiti katika kujiendesha kitaalam na kisasa, kwani mpaka sasa imefanikiwa kumiliki basi lake la kusafirisha wachezaji na benchi la ufundi, inamiliki uwanja wake wa mazoezi na uwanja wa mechi, pia iko katika ujenzi wa ofisi yake mpya.

Suala hilo limekuwa likishindikana kwa vilabu vingi vikongwe hapa nchini kwa miaka mingi sasa na kutokana na hiki wanachokifanya, wametoa funzo kubwa kuwa kila kitu kinawezekana kufanyika endapo kutakuwa na mipango mizuri.

Ihefu SC inaongoza katika msimamo wa Ligi Daraja la Kwanza, kundi A mpaka kufikia Machi 8, ikiwa na pointi 36 baada ya kucheza michezo 17 ambapo imebakiza mechi tano kumaliza ratiba ya kundi hilo ili kupata nafasi ya kujua hata yake katika kufuzu Ligi Kuu Tanzania bara.

Unakumbushwa: Kunawa mikono yako kwa maji safi yanayotiririka na sabuni au tumia kitakasa mikono (Sanitizer) kila mara, ili kujikinga na virusi vya Corona.