Sunday , 22nd Dec , 2019

Serikali imeeleza dhamira yake ya kukarabati vyuo vyote vya kilimo nchini ili kukabiliana na changamoto zinazovikabili vyuo hivyo ambapo ni pamoja na uchache na uchakavu wa vitendea kazi kama maabara, vifaa vya TEHAMA, na zana za kilimo yakiwemo matrekta.

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo tarehe 21 Disemba 2019 wakati alipotembelea Chuo cha Kilimo cha Uyole (MATI Uyole) wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Mbeya.

Ameeleza kuwa dhamira ya kukarabati vyuo hivyo imetokana na kujionea uchakavu wa miundombinu ikiwemo barabara, mifumo ya maji, majengo (Mabweni na nyumba za watumishi) katika chuo hicho pamoja na vyuo vingine vya kilimo.

Amesema kuwa serikali itakarabati vyuo hivyo ili kuwa na vyuo vya kisasa vinavyopendeza na vitakavyokuwa chachu ya kupata wataalamu waliokomaa kupitia mitaala iliyoboreshwa na zana bora za kilimo.

Pia, Mhe Hasunga amesema kuwa ili kuwa na wataalamu waliobobea vizuri kwenye sekta ya kilimo wizara yake imekusudia kuongeza muda wa mafunzo kwa vitendo (Field) kufikia mwaka mmoja kwani kufanya hivyo kutaongeza msukumo na kumjengea uwezo mkubwa mwanafunzi.

Tutafanya hivyo ili kuona alichojifunza mwanafunzi kama kina akisi weledi katika jamii na kama wazo hilo likikubalika tutarekebisha mitaala yetu ya kufundishia katika vyuo vyote vya kilimo na vyuo vikuu” Alikaririwa Mhe Hasunga