Saturday , 19th Oct , 2019

Waziri wa Katiba na Sheria Dkt Augustine Mahiga, amesema kuwa kompyuta zilizopo kwenye ofisi ya DPP hazijaibiwa, bali kilichoibiwa ni vipande vya Kompyuta kutoka ofisi ndogo ya mkoa na kwamba nyaraka zote za wahujumu uchumi, waliokiri na wanaoendelea kukiri makosa yao ziko salama.

Waziri wa Katiba na Sheria Dkt Augustine Mahiga

Waziri Dkt Mahiga amesema hayo leo Oktoba 19, 2019, wakati akitoa taarifa juu ya ugeni wa Mawaziri unaotarajiwa kuwasili nchini, kuanzia Jumatatu ya Oktoba 21, utakaohusisha wananchama 48 wa Afrika na Asia.

''Ukweli ni kwamba, ofisi ambayo ilivunjwa na baadhi ya vipande vya kompyuta kuchukuliwa ni katika ofisi ya Mkoa wa Dar es Salaam na Ofisi ya DPP haikuguswa, nyaraka zote zipo, taarifa zote zipo na kazi yake inaendelea, katika ile ofisi ndogo iliyopo Mkwepu Street Polisi bado wanaendelea na uchunguzi, Ofisi ya DPP na nyaraka zote alizonazo na anazifanyia kazi hazijaguswa, kitendo cha uhalifu hakijaathiri kaabisa uwezo wake na kumbukumbu tulizonazo kuhusu matatizo ya uhujumu uchumi'' amesema Dkt Mahiga.

Taarifa za madai ya wizi wa Kompyuta hizo, zilizokuwa na nyaraka muhimu za mafisadi zilianza kusambaa mwishoni  mwa wiki hii, ambapo jana Oktoba 18, 2019, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alithibitisha kutokea kwa wizi huo.