Friday , 20th Sep , 2019

Afisa Habari mpya wa Yanga, Hassan Bumbuli amesema kuwa hakutakuwa na mgongano wa majukumu kati yake na Afisa Mhamasishaji wa klabu hiyo, Antonio Nugaz.

Picha ya kushoto, Hassan Bumbuli (katikati) akiwa na Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao (kushoto) na mdau wa soka.

Maafisa hao wametangazwa jana na Mwenyekiti wa klabu hiyo, Dkt. Mshindo Msolla pamoja na Kamati ya Utendaji ikiwa ni mwezi mmoja tangu kutangazwa kwa nafasi hizo.

Akizungumza na EATV & Radio Digital, Hassan Bumbuli amesema kuwa kazi yake yeye ni kutoa taarifa rasmi za klabu kwenda kwa jamii ya soka, ikiwa ni pamoja na mashabiki, shirikisho la soka TFF, CAF pamoja na FIFA, wakati Antonio Nugaz yeye atakuwa akihusika na hamasa kwa wanachama.

"Uzuri ni kwamba kila kitu kimewekwa wazi tangu nafasi zilipotangazwa, mimi majukumu yangu hayatoingiliana kabisa na yake. Mimi nitakuwa natoa taarifa rasmi kwa watanzania na watu wa mpira na yeye atakuwa anafanya kazi ya hamasa, lakini mpango wake hautokuwa kama Manara, kwa sababu ile ni Simba na hii ni Yanga", amesema.

"Kuhusu mikakati yangu mipya, nimepanga kuibadilisha Yanga hasa katika kutoa habari katika mitandao ya kijamii. Yanga imekuwa nyuma kwenye hilo lakini na sasa mtaanza kuona vitu vipya", ameongeza.

Aidha Afisa Habari huyo ameeleza maandalizi yao kuelekea mchezo wa marudiano wa Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Zesco ambapo timu na mashabiki wataondoka nchini Septemba 25.