Tuesday , 2nd Jul , 2019

Habari iliyopo sasa ni juu ya michuano ya AFCON, ambapo timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' imeaga hapo jana baada ya kukamilisha ratiba ya makundi kwa kufungwa 3-0 na Algeria.

Timu ya taifa 'Taifa Stars'

Ni ukweli ulio wazi kuwa Stars haikutegemewa kufanya makubwa katika michuano hiyo lakini hakikuwa kigezo cha kushindwa kufanya hivyo kwani zipo timu ambazo zimeweza na ni mashindano yao ya kwanza katika historia ya nchi zao, mfano mzuri ukiwa ni Madagascar.

Timu ya taifa ya Madagascar imeonekana kuwashangaza wengi katika michuano hii kutokana na kiwango walichokionesha mpaka sasa, imefuzu hatua ya 16 bora na kuongoza kundi lake kwa pointi 7 baada ya kushinda michezo miwili na sare moja, ikimfunga Nigeria katika mchezo wa mwisho wa makundi ikiwa ni kwa mara ya kwanza kushiriki michuano hiyo.

Rais wa Shirikisho la Soka Afrika CAF, Ahmad Ahmad ambaye pia ni rais wa Shirikisho la Soka la Madagascar, amekuwa na msaada mkubwa katika mafanikio hayo, kutokana na sera yake ya kuruhusu wachezaji mbalimbali wa kigeni wenye asili ya nchi hiyo, hasa wanaochezea nchi za Ulaya kama Ufaransa kuja kuchezea timu ya taifa, baada ya kuona kuwa ligi ya nchi hiyo haina ubora wa kutoa wachezaji wanaoweza kuunda kikosi cha ushindani.

Kwa upande wa Uganda yenyewe imeamua kusimamia msingi yake ya kuendeleza vipaji vyao, ambapo imechagua kudumu na wachezaji wake zaidi ya asilimia 80 ya walioshiriki michuano iliyopita ya AFCON nchini Gabon mwaka 2017. Wachezaji wengi wanafahamiana kwa muda mrefu, jambo ambalo linawapa nguvu zaidi iliyowasiadia kufuzu hatua ya 16 mora mwaka huu.

Naye mchambuzi mkongwe wa masuala ya michezo nchini, Mwl Alex Kashasha amesema, "miongoni mwa mambo ambayo yameigharimu Taifa Stars katika michuano ni pamoja na uzoefu mdogo, lingine ni uoga wa kuhisi kuwa wanacheza na timu kubwa na utofauti wao katika matumizi ya mbinu lakini nimewaona wachezaji wamepambana sana. Ninaamini sote kama nchi lazima tufanye utafiti wa kutosha wenzetu walipofika ili nasi tupite humo, tunahitaji utendaji zaidi kuliko kuzungumza".