Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Profesa Makame Mnyaa Mbarawa.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano Sayansi na Teknolojia, Bw. John Mngondo amesema majadiliano hayo yanayoshirikisha ofisi ya Umoja wa Mataifa inayojishughulisha na udhibiti wa uhalifu wa mtandao yataleta suluhisho la athari zitokanazo na matumizi mabaya ya mitandao.
Aidha, Mngondo amesema kuwa serikali kwa kutambua umuhimu wa mawasiliano kwa njia ya mtandao imejidhatiti katika uboresha miundombinu ya mkongo wa taifa kwa zaidi ya kilometa 7,560 katika ngazi ya mikoa, huku lengo likiwa ni kufikia katika ngazi zote za wilaya na vijiji.
Kauli hiyo imekuja wiki chache baada ya wizara ya Sayansi na Teknolojia kueleza kuwa imekamilisha uandaaji wa miswada mitatu ya sheria zinazosimamia matumizi sahihi na salama ya huduma za mawasiliano ya mitandao.
Waziri wa Sayansi na Teknolojia Profesa Makame Mbarawa Mnyaa ameitaja miswada hiyo kuwa ni ule unaosimamia taarifa za siri za watumiaji wa huduma za mtandao, muswada wa sheria ya malipo na matumizi ya fedha kwa njia ya mtandao pamoja na sheria ya matumizi sahihi ya mawasiliano ya mtandao.
Kwa mujibu wa waziri Mnyaa, sheria hizo tayari zimepelekwa Baraza la Mawaziri kwa ajili ya kuzijadili na hatimaye zifikishwe bungeni ili nako zijadiliwe na zipitishwe kuwa sheria.