Tuesday , 12th Aug , 2014

Kampuni inayofanya utaifiti wa mafuta na gesi nchini Tanzania ya Swala Tanzania imekuwa kampuni ya kwanza kujisajili katika masoko ya hisa baina ya makampuni yanayojishughulisha na utafiti wa mafuta na gesi katika Afrika Mashariki.

Mkurugenzi Mkuu wa Swala Tanzania, Abdullah Mwinyi (katikati) akizungumza katika moja ya mikutano iliyoitishwa na kampuni hiyo hivi karibuni.

Afisa kutoka mamlaka ya masoko ya hisa na mitaji Bi. Grace Rubambey amesema hayo leo katika hafla ambapo kampuni hiyo ilianza rasmi kuuza hisa na kufanya biashara katika soko la hisa la Dar es Salaam.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Swala Tanzania Bw. David Mestres Ridge amesema kampuni hiyo imeweka historia kwa kuvuka malengo ya kuuza hisa zake na kufanikiwa kukusanya fedha za Tanzania shilingi bilioni 6.64 kati ya shilingi bilioni 4 ilizotegemea kukusanya hapo awali.

Wakati huo huo, wizara ya ujenzi nchini Tanzania imepanga kutumia fedha za Tanzania shilingi trilioni moja kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali inayolenga kuboresha usafirishaji na kupunguza foleni kwa jiji la Dar es Salaam.

Waziri wa wizara hiyo Dkt John Pombe Magufuli, amesema hayo jijini Dar es Salam na kutaja baadhi ya miradi kuwa ni barabara ya Mwenge Tegeta, daraja la Kigamboni pamoja na barabara kadhaa kwa ajili ya kuondoa msongamano wa magari katikati ya jiji.

Aidha, katika miradi hiyo Dkt Magufuli amesema ipo pia miradi ya ujenzi wa barabara za juu katika baadhi ya makutano ya barabara zenye msongamano mkubwa na kwamba hatua hiyo italisaidia taifa kupunguza hasara za kiuchumi zinazotokana na msongamano wa magari.