Tuesday , 28th Aug , 2018

Spika wa Bunge nchini Uganda, Rebecca Kadaga,  amemwandikia barua Rais Yoweri Museveni akimtaka achukue hatua za haraka za kukamatwa na kushtakiwa maofisa usalama waliohusika kuwapiga na kuwatesa wabunge na wanahabari siku ya kuhitimisha kampeni za uchaguzi mdogo Manispaa ya Arua.

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni.

Katika barua yake aliyoandika jana Agosti 27, Kadaga amemwambia Museveni kwamba maafisa usalama kutoka Kamandi Maalumu ya Ulinzi (SFC - kikosi cha kumlinda Rais), polisi na wanajeshi ambao waliwapiga wabunge na raia ambao hawakuwa na silaha, hivyo wanatakiwa wakamatwe na washtakiwe mahakamani haraka iwezekanavyo.

Barua hiyo ilisisitiza kuwa ,“Kama hili halitafanyika, itakuwa kazi ngumu kuendesha shughuli za serikali bungeni. Bunge haliwezi kupuuza wala kusamehe vitendo vya utesaji”.

Siku ya kufunga kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge katika Manispaa ya Arua, Mbunge wa Kyadondo Mashariki, Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine,na wabunge wengine wa upinzani akiwemo mshindi Kassiano Wadri, Francis Zaake (Mityana), Paul Mwiri (Jinja Mashariki), Gerald Karuhanga (Ntungamo) na Mike Mabikke (mbunge wa zamani wa Makindye wa zamani wa Makindye Mashariki) walikamatwa na maafisa wa polisi na jeshi wakituhumiwa kurushia mawe na kuvunja kioo cha gari la msafara wa Rais.

Katika vurugu hizo aliuawa dereva wa Bobi Wine na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya wanajeshi maalumu wanaomlinda Rais kuwashambulia watu kwa madai walihusika kupiga jiwe na kuvunja kioo cha gari la msafara wa Rais.