Monday , 7th Jul , 2014

Baraza la maaskofu katoliki Tanzania (TEC), limetoa tamko zito kwa wajumbe wa Bunge Maalum la kat

Baadhi ya wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) wakijadiliana moja ya vipengele tata kwenye rasimu ya pili ya katiba.

Baraza la maaskofu katoliki Tanzania (TEC), limetoa tamko zito kwa wajumbe wa Bunge Maalum la katiba, likiwataka wawe wa moja na kufanya kazi yao kwa mtazamo usioegemea siasa za vyama.

Katika tamko hilo la Mwezi Juni mwaka huu, lililosainiwa na Rais wa TEC, Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa na kusoma kwenye ibada za kanisa hilo nchini kote hapo jana, wajumbe hao wanakumbushwa kuwa yeyote anayedharau hitaji la Katiba mpya na anayejaribu kupuuza na kuweka kando rasimu ya pili, huyo si muwakilishi wa watu na kwamba, mwisho wake historia itamuhukumu.

Pia waliwasihi wajumbe wa katiba kurejea katika sehemu ya Pili ya Mjadala Agosti mwaka huu, wakiwa na moyo na mtazamo mpya, waache ubinafsi na makundi.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, chama cha upinzani cha TADEA, kilitoa wito wa kuutaka umoja wa katiba ya wananchi UKAWA kurejea katika bunge maalumu la katiba ili kukamilisha mchakato wa kuwapatia Watanzania katiba mpya.

Katibu mkuu wa chama hicho ambaye pia ni mjumbe wa bunge maalumu la katiba Bw. Juma Ali Khatib, ametoa wito huo ikiwa zimebakia siku chache kabla ya kuanza kwa vikao vya bunge hilo ambavyo vilisitishwa kwa muda kupisha bunge la bajeti.

Bw. Khatib amesema hoja wanazozitoa wajumbe wa UKAWA ni za msingi ambazo hata yeye anaziunga mkono lakini njia inayotumiwa na wajumbe hao kutoka vyama vya CUF na Chadema sio sahihi kwani suluhu haifikiwi tofauti zinaweza kupatikana ndani ya bunge hilo na hata kwa njia ya mazungumzo.